KUPATA ASILIMIA 100% KATIKA MITIHANI MIGUMU

Kupata 100% Katika Mtihani Mgumu

Kichwa kinachoonekana hapa, ndicho ninachoona kuwa kinastahili, kubebwa na maandiko ya leo. Huenda wakati tukio hili, tayari Isaka alikuwa na umri wa miaka isiyopungua 15.

WITO ULIOBEBA OMBI GUMU (1-2)
Moja ya mambo ya kufurahisha tunayokutana nayo katika maisha ya Ibrahimu, ni jinsi alivyokuwa akiisikia sauti ya Mungu mara kwa mara. Kuongea huku kulimwezesha kumtambua kama Mungu, pia kumtambua kama Baba, anayetambua umuhimu wa sauti yake kwa watoto wake.

Katika kusikia sauti ya Mungu katika maandiko haya, Ibrahimu alipewa mtihani (nacah-Kiebrania) nacah ambayo ni ngumu kuliko nacah zote alizowahi kuzipokea huko nyuma. Nacah ya kwanza ngumu kuipokea, ni ile iliyomtaka kuondoka katika nchi na jamaa yake, kwenda kuanzisha maisha katika nchi ya kigeni. Nacah iliyofuata kwa ugumu, ilikuwa ni ile ya kumfukuza Hajiri pamoja na Ishmaeli. Tunachojifunza hapa, ni kuwa Mungu huwa hasemi nasi kila wakati, kwa kutumia maneno yaliyobeba mionjo ya karamu.

UTII WA KUSTAAJABISHA (22:3)
INGAWA zamu hii Mungu alimjia Ibrahimu na mtihani ambao hakuwa amejiandaa nao, Ibrahimu alikubali kwa haraka kuufanya. Siku Mungu alipoongea naye, kesho yake alfajiri safari ilianza ya kuendea chumba cha mtihani, nchini Moria. Nchi ya Moria inayozungumziwa hapa, ilihusisha milima inayozunguka Yerusalemu, ikiwemo ile ya mlima wa mizeituni, Sayuni, Moria na Kalvari. Kilele cha mlima Kalvari ndicho kilichokuwa kirefu, kuliko vile vya milima mingine. Waalimu wengi akiwemo Finis Jennings Dake, wanaamini kuwa kilima hiki ndipo mahali Ibrahimu alipofanyia mtihani wake.

Uharaka wa kutendea kazi sauti ya Mungu, ni uthibitisho wa wazi unaoonesha utayari wa Ibrahimu, katika kuitii sauti ya Mungu. Mara zote kiwango chetu cha kumpenda Mungu, kinaonekana katika uharaka wetu, wa kutendea kazi neno lake.

KANUNI YA CHUMBA CHA MTIHANI (22:4-5)
Ingawa hatusomi mahali ambapo Ibrahimu alielekezwa na Mungu kuhusu watu wa kuandamana naye katika eneo la kufanyia mtihani wake, anaonekana kuelewa kanuni zinazotakiwa kufuatwa, wakati wa kuingia katika chumba cha mtihani. Moja ya kanuni hizi, ni kutoingia na mtu mwingine. Kwa kuelewa hili, alilazimika kuwaacha watumishi pamoja na punda wake!

Ukweli ambao kila mwamini anatakiwa kuuelewa ni kuwa ingawa Mungu ameweka watumishi katika kanisa kwa lengo la kuandaa waamini, mitihani ya kimaisha itakapotokea, mwamini ataingia peke yake katika chumba cha mtihani. Suala la maandalizi ni la kanisa nzima, ila mtihani ni wa mtu binafsi! Kwa kutotambua ukweli huu, waamini wengi wanaishia kukwazika na kurudi nyuma, pale wanapowakosa waliokuwa wakiwafunza katika mitihani wanayopitia. Nasema mitihani (nacah), sizungumzii mashambulizi yanayotoka kwa mwovu.

MWANA ALIYEPATA MALEZI MEMA (22:5-8)
Wakati wawili hawa Ibrahimu na mwanawe walipokuwa wakielekea katika eneo la mtihani, Isaka alimwuliza baba yake swali. Ingawa kwa nje swali hili lilikuwa rahisi, ndani ya moyo wa Ibrahimu ulikuwa ni msumari wa moto. “Baba, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa?”

Swali hili linaonesha aina ya malezi ambayo Isaka alikuzwa nayo. Kama angekuwa kijana baradhuli, ni wazi asingeuliza swali hili. Hapa tunajifunza mambo matatu kuhusiana na mwana aliyelelewa vizuri. Jambo la kwanza, humlinda mzazi wake kiroho. Kwa kuwa Isaka alikuwa ndiye sadaka iliyokuwa ikienda kutolewa, tunajifunza kuwa sadaka nzuri ni sadaka iliyo uhai na inayozungumza. Jambo la tatu ni kuwa sadaka njema, huwa inamkumbusha Mungu mambo ambayo anayeitoa, anadhania kuwa Mungu ameyasahau.

Kwa kutambua matukio yaliyokuwa mbele yao, Ibrahimu aliamua kumpatia Isaka jibu lililokuwa kinyume na ukweli uliokuwa moyoni mwake. Kwa kuwa tayari alikuwa na sadaka, alikuwa hana jibu lingine zaidi ya lile alilolitoa. Angesema “Tunayo mwanangu,” Isaka angeuliza kuwa “Iko wapi baba?” Hivyo alichagua kutoa jibu linaloonekana kama danganya toto, ila kwa ndani alikuwa anasema kuwa “sadaka ipo!”

KUFAULU KWA IBRAHIMU (22:9-12)
Kuna mambo machache ya kuzungumza hapa, kuhusiana na jinsi Ibrahimu alivyofaulu mtihani wake. Jambo la kwanza, ni kuhusu jukumu la msingi la mtoaji wa sadaka. Ingawa Ibrahimu alikuwa na sadaka ya kumtolea Mungu, malaika hawakushuka kumjengea mahali pa kutolea sadaka yake. Badala yake, yeye mwenyewe alilazimika kujenga mahali pa kutolea sadaka yake. Waamini wote wa kanisa la mahali, wanatakiwa kuelewa ukweli huu. Wao ndio wanaotakiwa kujitolea kumjengea Mungu nyumba, watakayoitumia kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka zao za mali, sifa au shukrani.

Jambo la pili, tunalokutana nalo katika maandiko haya, ni utii wa Isaka. Kwa kuwa alikuwa kijana asiyepungua miaka 15, angeliweza kuleta vurugu wakati wa kufungwa, tayari kuwekwa juu ya kuni. Cha kustaajabisha ni kuwa jambo hili, halikutokea. Mara zote mtoto aliyefunzwa vizuri ni mtii kwa baba yake, hata katika masuala magumu yaliyofichika machoni pake.

Jambo la tatu la kujifunza, linaendana na kijana ambaye Ibrahimu aliagizwa na Mungu amtoe kama sadaka. Mpaka kufikia hatua hii, Ibrahimu alikuwa amejaliwa na Mungu kuwa na vijana wawili, ambao ni Ishmaeli na Isaka. Ingawa Ishmaeli alikuwa amefukuzwa, bado wanaendelea kuwasiliana. Nasema hivi kutokana na ukweli kuwa wakati wa mazishi yake, wote wawili Isaka na Ishmaeli walishirikiana kumzika.

Ingawa vijana hawa walikuwa ni wa thamani mbele za Mungu, walikuwa na hadhi tofauti kuhusiana na mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu. Hali kadhalika Isaka alikuwa amekamata moyo wa Ibrahimu, kuliko ilivyokuwa kwa Ishmaeli. Kwa kuwa Mungu alimwagiza Ibrahimu amtoe Isaka badala ya Ishmaeli, unapofika wakati wa kujitolea na kutoa katika ufalme wa Mungu, hatutakiwi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *